PSSSF YAFIKIA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM TANGA
Tanga, Julai 28, 2026
Katika kuendeleza dhamira yake ya kuchangia maendeleo ya jamii kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSI) chini ya kampeni yake ya #PSSSFKaribuNaJamii, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekabidhi rasmi mradi wa miundombinu wenye thamani ya Shilingi milioni 25 katika Shule ya Msingi Majani Mapana iliyopo mkoani Tanga.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa chumba cha darasa, chumba cha mapumziko pamoja na vifaa mbalimbali vya michezo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum.

Baadhi ya watumishi wa Psssf, walimu na viongozi wa kata ya Nguvumali, Manispaa ya Tanga, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya hafla ya kukabidhi mradi wa miundombinu uliojengwa na Psssf kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya Msingi Majani Mapana, Tanga
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Bw. Kwame Temu alieleza kuwa msaada huo unalenga kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata haki yao ya msingi ya elimu. Alisisitiza kuwa hatua hiyo itawasaidia wanafunzi hao kujifunza katika mazingira yanayowawezesha kujifunza kwa ufanisi, kushiriki katika michezo na kukuza vipaji vyao mbalimbali.

Afisa Elimu Shule za Awali na Msingi mkoa wa Tanga Ndugu Shomari Bane (mwenye suti ya kijivu) pamoja na Meneja wa Psssf wa Kanda ya Kaskazini Mashariki (Mwenye suti ya bluu) wakifuatilia maelezo wakati wakukagua mradi wa miundombinu kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum shule ya Majani Mapana Tanga
Kwa upande wake, Afisa Elimu Kata ya Nguvumali, Bi. Lilian Shetui, aliishukuru PSSSF kwa mchango huo akieleza kuwa miundombinu hiyo itaongeza ubora wa huduma za elimu shuleni hapo. Kwa niaba ya Afisa Elimu Shule za Awali na Msingi wa mkoa huo, Bi. Lilian alipongeza PSSSF kwa kuona umuhimu wa kundi hilo na kutoa msaada utakaokuwa na tija kubwa kwa watoto hao.

Baadhi ya Wanafunzi katika shule ya Msingi Majan Mapana wenye uhitaji maalum wakicheza kwa furaha katika vifaa vya michezo vilivyofadhiliwa na PSSSF.
Kupitia mchango huo, jumla ya wanafunzi 71 wenye mahitaji maalum na usonji katika Shule ya Majani Mapana wanatarajiwa kunufaika na mazingira rafiki ya kujifunzia, kupumzika na kucheza, hatua inayochochea elimu jumuishi na kuwajengea msingi bora wa maisha ya baadaye.