Coat of Arms

PUBLIC SERVICE SOCIAL SECURITY FUND

Leo. Kesho. Pamoja.

PSSSF Logo
WAAJIRI WA SEKTA YA UMMA WAKUMBUSHWA KUWASILISHA MICHANGO YA WATUMISHI KWA WAKATI

WAAJIRI WA SEKTA YA UMMA WAKUMBUSHWA KUWASILISHA MICHANGO YA WATUMISHI KWA WAKATI

News
News

Sabasaba, Julai 13, 2026


Waajiri katika Sekta ya Umma wamekumbushwa kutekeleza wajibu wao wa kisheria wa kuwasilisha michango ya watumishi kwa wakati katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), ili kuhakikisha wanachama wanapata stahiki zao kwa wakati wanapostaafu.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa PSSSF, Bi. Hilda Nkunna, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye Viwanja vya Julius Nyerere.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa PSSSF, Bi. Hilda Nkunna (kushoto), akitoa elimu kwa Mratibu wa Kituo cha Mafunzo na Utafiti cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwanachama wa PSSSF, Profesa Herbert Qambalo, kuhusu huduma zitolewazo na Mfuko, kwenye banda la Mfuko katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam


Bi. Nkunna amesema pamoja na waajiri kutimiza wajibu wao, ni muhimu pia kwa watumishi kuwa na utamaduni wa kufuatilia taarifa za michango yao mara kwa mara ili kujiridhisha kuwa michango yao inawasilishwa kwa usahihi na kwa wakati.

Akizungumzia kampeni ya Mfuko ya "Tunalipa Jana", amesema lengo lake ni kuhakikisha Mwanachama anapowasilisha nyaraka zote muhimu kwa ukamilifu analipwa mafao yake pindi tu anapostaafu.

Mkurgenzi wa Huduma za Sheria, Mfuko wa PSSSF, Bi. Hilda Nkunna (kushoto), akimsikiliza Afisa Uhusiano wa PSSSF, Bi. Queen Edward kuhusu ufanisi wa Meza Janja (Smart Table) inavyohudumia wanachama kidijitali, kwenye Banda la Mfuko, katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendela kwenye Viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.


Ameeleza kuwa maendeleo ya teknolojia yameiwezesha PSSSF kurahisisha utoaji wa huduma, ambapo kwa sasa wanachama wanaweza kupata huduma nyingi kidijitali bila kulazimika kufika ofisini.

"Mwanachama anaweza kufuatilia taarifa zake kupitia programu ya PSSSF Kiganjani, kutumia PSSSF Member Portal, au kutembelea ofisi zetu zilizopo kote nchini, Tanzania Bara na Zanzibar," amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha Mafunzo na Utafiti cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwanachama wa PSSSF, Profesa Herbert Qambalo, amepongeza hatua ya Mfuko kutumia mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma.

"Nimefurahishwa sana na matumizi ya teknolojia. Kupitia mfumo huu, nimeweza kuona mtiririko wa michango yangu tangu nilipoajiriwa, kiwango kinachochangiwa na mwajiri pamoja na mchango wangu binafsi. Hii inaongeza uwazi na kuimarisha imani ya wanachama kwa Mfuko," amesema Prof. Qambalo.

Naye Mwalimu Maombi Kyando kutoka Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, amesema matumizi ya huduma za kidijitali za PSSSF yamerahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa PSSSF, Bi. Hilda Nkunna (kushoto), akimkabidhi mfuko wenye machapisho mbalimbali yenye kutoa elimu kuhusu shughuli za PSSSF, Mratibu wa Kituo cha Mafunzo na Utafiti cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwanachama wa PSSSF, Profesa Herbert Qambalo, kwenye banda la Mfuko katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea kwenye Viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam