Coat of Arms

PUBLIC SERVICE SOCIAL SECURITY FUND

Leo. Kesho. Pamoja.

PSSSF Logo
MBUNGE WA ILEMELA ASIFU MAPINDUZI MAKUBWA YA UTOAJI HUDUMA PSSSF

MBUNGE WA ILEMELA ASIFU MAPINDUZI MAKUBWA YA UTOAJI HUDUMA PSSSF

News
News

Sabasaba, Julai 14, 2026

Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Kafiti Kafiti, ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa mageuzi makubwa yaliyofanyika katika utoaji wa huduma kwa wanachama wake.

Mhe. Kafiti alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la PSSSF katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere.

Alisema PSSSF imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma, jambo linalodhihirishwa na utekelezaji wa kaulimbiu yake ya "Tunalipa Jana."

"PSSSF ya leo siyo ile ya zamani. Nimefurahishwa kuona huduma zimeendelea kuboreshwa. Walipofika kwenye Kamati walitueleza kuhusu kaulimbiu ya 'Tunalipa Jana', na leo nimejionea mwenyewe kuwa kweli wanalipa jana," alisema Mhe. Kafiti.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Kafiti Kafiti (kulia), akipokea mfuko wenye majarida na vipeperushi vyenye taarifa za Mfuko, kutoka kwa Afisa wa PSSSF, Bi. Neema Lowassa, alipotembelea banda la Mfuko kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam


Aidha, alieleza kufurahishwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Mfuko katika mifumo ya kidijitali na teknolojia, ambao umeongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuwawezesha wanachama kupata huduma kwa urahisi bila kulazimika kufika katika ofisi za PSSSF.

Mhe. Kafiti alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Fortunatus Magambo, pamoja na watumishi wote wa Mfuko kwa juhudi wanazoendelea kuzifanya katika kuboresha huduma na kuimarisha ustawi wa wanachama.

"Ninyi mmeshikilia taifa hili. Wote tunaofanya kazi safari yetu ni kuelekea uzeeni, hivyo kila mmoja wetu atahitaji huduma za PSSSF wakati wa kustaafu. Hongereni kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya," alisisitiza.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Kafiti Kafiti (wanne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wakiongozwa na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw. Omega Ngole (wa kwanza kulia), alipotembelea banda la Mfuko kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.