BODI YA ZABUNI PSSSF YAKAGUA UJENZI WA MOUNT KILIMANJARO JIJINI ARUSHA. *Yaridhishwa na Kasi na ujenzi *Utakuwa kitovu cha utalii, mikutano
Bodi ya zabuni ya Mfuko wa PSSSF, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Bw. Erick Kato imetembelea mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mount Kilimanjaro International Convention Centre (MKICC) jijini Arusha, Novemba 25, 2026, ili kujionea Maendeleo ya ujenzi.

Mhandisi Mshauri wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mount Kilimanjaro International Convention Centre (MKICC), Mhandisi Iddi Mvungi (wakwanza kulia), akiwaongoza wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya PSSSF wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho jijini Arusha, Novemba 25, 2026.
Akizungumzia maendeleo ya mradi huo Bw. katto alisema," kwa kweli ukifika hapa unaona kazi kubwa inafanyika kwa Kasi na weledi, ni matumaini yetu kila kitu kipo sawa na utakamilika kama ilivyopangwa".

Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Eric Kato (wa pili kulia), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa bodi hiyo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mount Kilimanjaro International Convention Centre (MKICC), jijini Arusha, Novemba 25, 2026.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Mradi huo, Bw. Iddi Mvungi alisema mradi huo unaendeshwa kwa ubia kati ya PSSSF na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) unatarajiwa kuwa kitovu cha utalii, biashara na mikutano ya kimataifa.

Muonekano wa moja ya majengo yanayojengwa katika mradi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mount Kilimanjaro International Convention Centre (MKICC), jijini Arusha, Novemba 25, 2026.
"Mradi huu upo katika mfumo wa kijiji cha utalii kitakachojumuisha maeneo manne makuu yanayoakisi utajiri wa vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania", alifafanua Mha. Mvungi.
Alisema, miongoni mwa miundombinu itakayojengwa ni ukumbi mkubwa wa mikutano wenye matumizi mbalimbali (Multipurpose Conference Hall), utakaokuwa na uwezo wa kuhudumia washiriki kati ya 10,000 kwa wakati mmoja. Ukumbi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa Tanzania kuvutia na kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa.
Muonekano wa moja ya majengo yanayojengwa katika mradi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mount Kilimanjaro International Convention Centre (MKICC), jijini Arusha, Novemba 25, 2026
Aidha, Mha. Mvungi aliweka wazi kuwa mradi huo utakuwa na eneo la maduka makubwa (Shopping Mall) litakalotoa huduma mbalimbali za kibiashara, hoteli ya hadhi ya nyota tano yenye vyumba 340, kwa ajili ya kuwahudumia wageni na washiriki wa mikutano watakaotembelea kituo hicho wakiwemo marais, ukumbi wa maonyesho wenye ukubwa wa mita za mraba 20,000 na jengo la ofisi lenye ukubwa wa mita za mraba 2600.