RAS GEITA: WAAJIRI WASILISHENI NYARAKA NA MICHANGO KWA WAKATI ILI PSSSF “WALIPE JANA”
Na Mwandishi wetu, Geita
Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Mohamed Jumanne Gombati, amewataka waajiri mkoani humo kutunza nyaraka za watumishi na kuwasilisha michango kwa usahihi na kwa wakati, ili kuuwezesha Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kutekeleza dhamira yake ya “Tunalipa Jana” ya kumlipa mstaafu mafao siku moja kabla ya tarehe yake ya kustaafu.
Akifungua semina ya PSSSF kwa wanachama na waajiri wa Mkoa wa Geita iliyofanyika Oktoba 8, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano Otonde, Bw. Gombati alisema Wakuu wa Idara za Utumishi na Utawala, Maafisa Utumishi na Wahasibu ndio kiungo kati ya mtumishi na Mfuko. “Ninyi ni mabalozi na daraja kati ya watumishi na PSSSF. Tunzeni nyaraka za watumishi wenu, wasilisheni michango kwa usahihi na kwa wakati, ili kuwawezesha PSSSF kulipa jana,” alisema Katibu Tawala.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Mohamed Gombati akizungumza katika semina ya PSSSF kwa maafisa Rasilimaliwatu wa mkoa wa Geita iliyofanyika mapema leo Oktoba 8, 2026 ikiwa na lengo la kuwaelimisha kuhusu huduma mbalimbali zitolewazo na Mfuko.
Bw. Gombati aliipongeza PSSSF kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema yanaendana na msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kutumia mifumo ya kisasa. Aliwataka washiriki kuwahimiza wanachama na wastaafu kufuatilia taarifa zao kupitia mifumo ya kidijitali ya Mfuko na maafisa wa PSSSF kuhakikisha mafunzo yanakuwa shirikishi na yanajibu changamoto halisi za wanachama.

Washiriki wa semina ya PSSSF kwa maafisa Rasilimaliwatu na Utawala wakifuatilia mada katika semina hiyo
Akiunga mkono kauli hiyo, Meneja wa PSSSF Kanda ya Ziwa Magharibi, Bw. Thomas Labi, alisema mafanikio ya “Tunalipa Jana” yanatokana na ushirikiano wa mwanachama, mwajiri na Mfuko, na kwamba maandalizi ya kustaafu huanza siku ya kwanza ya ajira, hivyo waajiri wanapaswa kuwasajili watumishi wapya ndani ya siku 30 tangu kuajiriwa. “Mwajiri anapohakiki madai kwa wakati, anauwezesha Mfuko kukamilisha malipo kwa wakati. Uhakiki unapochelewa, mchakato wa malipo unaweza pia kuchelewa,” alisema.

Picha ya pamoja Katibu Tawala Mkoa wa Geita na Meneja wa PSSSF Kanda ya Ziwa Magahribi, Bw. Thomas Labi wakiwa na maofisa wa PSSSF na washiriki wa semina ya PSSSF kwa maafisa Rasilimaliwatu na Utawala wa mkoa wa Geita.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu wa Halmashauri ya Wilaya Bukombe, Bi. Caroline Kayombo, akizungumza kwa niaba ya washiriki, aliishukuru PSSSF kwa kuandaa mafunzo hayo. “Niwashukuru sana PSSSF kwa kuandaa mafunzo haya hasa namna ya kutumia mifumo ya kidigitali. Kuna mambo nilikuwa nayaelewa tofauti, lakini baada ya mafunzo haya tutaenda kufanya vizuri zaidi. Kwa niaba ya wenzangu, niwashukuru sana kwa mafunzo haya,” alisema Bi. Kayombo. PSSSF inawahimiza wanachama na wastaafu kutumia PSSSF Member Portal na PSSSF Kiganjani kufuatilia taarifa zao na wanapokuwa na changamoto kupiga simu ya bure namba 0800110055.