MKURUGENZI MKUU PSSSF ASHIRIKI MKUTANO WA PILI WA DOHA DIALOGUE JIJINI DAR ES SALAAM
Dar es Salaam, Oktoba 6, 2026,
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Fortunatus Magambo, ameshiriki Mkutano wa Pili wa ‘Doha Dialogue’ unaohusu uhamaji wa nguvu kazi na ajira ambao umefunguliwa rasmi jijini Dar es Salaam na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Fortunatus Magambo (Wapili kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda,wakiwa katika ufunguzi wa kikao cha Makatibu Wakuu, Watendaji na Wataalamu wa Mkutano wa Pili wa Doha Dialogue kuhusu uhamaji wa nguvu kazi na ajira, leo Oktoba 5, 2026 jijini dar es ssalaam.
Mkutano huo wa siku mbili umefanyika Oktoba 5-6, 2026 katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, ukikutanisha viongozi, watendaji na wataalamu kutoka Tanzania, Qatar, Tume ya Umoja wa Afrika pamoja na nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (Gulf Cooperation Council – GCC+).
Kabla ya ufunguzi rasmi wa mkutano huo, kulifanyika kikao cha Makatibu Wakuu, Watendaji na Wataalamu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Nchi ya Qatar, Tume ya Umoja wa Afrika na washiriki kutoka nchi wanachama wa GCC+, ambapo Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Magambo, pia alishiriki.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Fortunatus Magambo (Wakwanza Kulia) akiwa na viongozi wenzake, katika ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa ‘Doha Dialoguie’ Jijini Dar Es Salaaam, Oktoba 6, 2026
Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya uhamiaji wa nguvu kazi, ajira na ulinzi wa haki za wafanyakazi, hususan katika kuhakikisha kuwa uhamaji wa nguvu kazi kati ya nchi za Afrika na nchi za GCC+ unafanyika kwa usalama, kwa kuzingatia haki za wafanyakazi na kwa manufaa ya pande zote.
Aidha, Serikali ya Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na nchi za GCC+ katika kulinda haki na maslahi ya wahamiaji, pamoja na kuweka mazingira bora yatakayowezesha uhamaji wa nguvu kazi kuwa salama, wenye haki na wenye tija.