
Bodi yaridhishwa na uwekezaji wa Mfuko
Mshauri wa Menejimenti ya kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro, Bw. Javad Sethi akitoa maelezo kwa wajumbe wa bodi juu uzalishaji wa ngozi kiwandani hapo.
*Mwenyekiti: Endeleeni kusimamia vyema miradi
*DG: Tujifunze kwa wataalamu wa kigeni
Na Mwandishi wetu, Moshi
Bodi ya wadhamini wa PSSSF wameutaka uongozi kuedelea kusimamia vyema uwekezaji wa mfuko katika maeneo mbalimbali nchini ili uwekezaji huo uwe wa tija kwa Mfuko na taifa kwa jumla.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bi. Joyce Mapunjo baada ya kuhitimisha ziara ya kutembelea miradi ya Mfuko iliyopo kanda ya kasikazini ambapo walitembelea kiwanda cha ngozi cha kimataifa cha Kilimanjaro (KLICL) kinachoendeshwa kwa ubia kati ya PSSSF na Jeshi la Magereza, mradi wa nyumba za makazi Oloirieni, jengo la biashara la PSSSF Arusha house na jengo la Gold Crest Hotel.
“Kiwanda hiki cha KLICL kikisimamiwa vyema kinaweza kutoa ajira kwa watu wengi wakiwemo vijana wetu, pia kikisimamiwa vizuri kitakuwa kiwanda cha mfano Afrika Mashariki.” Alisema Bi.Mapunjo.
Mshauri wa Menejimenti ya kiwanda cha bidhaa za ngozi cha Kilimanjaro, Bw. Javad Sethi akitoa maelezo kwa wajumbe wa bodi juu uzalishaji wa ngozi kiwandani hapo.
Mwenyekiti huyo alisema Mfuko kwa kushirikia na wabia wengine katika miradi inayoendeshwa na Mfuko wakutane kujadili changamoto kama zipo kwa lengo la kuhakikisha miradi inafanyakazi kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF aliwataka watanzania ambao wameajiriwa katika miradi ambapo kuna wataalam kutoa nje ya nchi, kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kuchukua utaalam kutoka kwa wataalamu hao ili wakiondoka wao ndio wawe waendeshaji wa miradi hiyo.
Mradi wa Oloirieni umefikia malengo ya uwekezaji kwa kurejesha gharama za mradi tangu mwaka 2012 na kuendelea kuwa kitegauchumi muhimu na chanzo cha mapato kwa Mfuko. Nyumba hizi zimekuwa kimbilio la wafanyakazi wa taasisi nyingi za kimataifa zenye makao makuu Jijini Arusha kwani zinaaminika kuwa sehemu salama zaidi na zenye huduma bora.
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Dkt. Rhimo Nyansaho akizungumza wakati bodi ya Wadhamini wa PSSSF walipotembelea kiwanda cha ngozi cha kimataifa cha Kilimanjaro. Katikati ni Mwenyeki wa Bodi, Bi. Joyce Mapunjo na kushoto ni Kaimu Mkugenzi Mkuu wa kiwanda hicho, Mha. Saiba Edward.
Awali kabla ya kutembelea miradi bodi ya wadhamini wa PSSSF ilifanya vikao vyake jijini Arusha. Wajumbe wa bodi hiyo ni; Bi. Joyce Mapunjo (Mwenyekiti), CPA. Pius Meneno (Makamu Mwenyekiti), Bi. Emma Lyimo, Dkt. Haphsa Hincha, Bw. Tumaini Nyamhokya, Bi. Suzanne Doran, Bi. Vicky Jengo, Bw. Sadi Shemliwa na Dkt. Rhimo Nyansaho (Katibu) ambaye pia Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF.