
KIWANDA CHA KLICL KITATENGENEZA FAIDA KUBWA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete akiangalia viatu vinavyotengenezwa na kiwanda cha KLICL cha Moshi mkoani Kilimanjaro.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Kiwanda cha Kimataifa cha Bidhaa za Ngozi Kilimanjaro (KLICL) ambacho kinamilikiwa kwa ubia kati ya Mfuko na Jeshi la Magereza kipo katika hatua nzuri.
Mhe. Waziri amesema hayo leo mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Serikali (PIC) walipotembelea kiwanda hicho kilichoko mjini Moshi. "Jukumu langu kubwa ni kuhakikisha kuwa mipango na malengo tuliyojiwekea yanafikiwa, niwahakikishie kuwa kiwanda kitakapofikia uzalishaji kwa asilimia 100 kitatengeneza faida kubwa na tutaondoa gharama nyingi na tutakua pazuri," alisema Mhe. Kikwete.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru aliwaambia wajumbe hao kuwa Mfuko una mkakati wa kuwekeza katika miradi tofauti, na kila mradi utazingatia kutoa huduma kwa jamii.
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul-Razaq Badru akuzungumza na Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Serikali (PIC) walipotembelea leo kiwanda cha KLICL.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Augustine Vumma Hole, alishauri kiwanda hicho kuboresha bidhaa wanazozalisha kuendana na wakati bila kuacha ubora. "Jitahidini sana mnyumbulike kwenye fasheni bila kuacha ubora unaotakiwa kitaifa na kimataifa, mpaka sasa mmefanya kazi nzuri." Alisema Mhe. Vuma.
Mhe. Vuma, pia alipongeza uzalishaji unaofanyika katika kiwanda hicho pia kuongeza uzalishaji ili kuhakikisha fedha zilizowekwa na Serikali katika mradi huu zirudi kwa wakati. Wajumbe wa Kamati hiyo walishauri kutafuta kampuni makubwa ya uzalishaji bidhaa za ngozi ili kushirikiana nao.
Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Serikali (PIC) kwenye picha ya pamoja na Uongozi wa PSSSF pamoja na Uongozi wa Kiwanda cha KLICL walipotembelea kiwanda hicho.