Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Ahudhuria Maadhimisho ya Wiki ya Tume ya Utumishi wa Umma
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi, akipokea cheti cha kutambua mchango wa Mfuko kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu Hamisa Hamisi Kalombola, wakati wa maadhimisho ya kilele cha wiki ya Tume ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma.
*Aahidi Ushirikiano na Kuboresha Huduma Kidijitali
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi, audhuria kilele cha maadhimisho ya wiki ya Tume ya Utumishi wa Umma tarehe 29 Septemba, 2024, jijini Dodoma, alitoa pongezi kwa Tume kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuboresha masuala ya utumishi wa umma. Aliahidi ushirikiano wa karibu kati ya PSSSF na Tume hiyo ili kuhakikisha watumishi wa umma wanapata haki zao kikamilifu, huku akisisitiza umuhimu wa taasisi hizo mbili kufanya kazi kwa pamoja.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi, akizungumza wakati wa maadhimisho ya kilele cha wiki ya Tume ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma,
Bw. Kijazi pia alielezea juhudi za PSSSF katika kuboresha huduma kwa wanachama wake kupitia matumizi ya teknolojia ya kidijitali. Alifafanua kwamba Mfuko umefanikiwa kusogeza karibu huduma kwa wanachama kwa njia ya kidijitali, hatua ambayo imeongeza ufanisi na kupunguza usumbufu Wanachama na Wastaafu.
“Sasa wanachama wanaweza kufuatilia michango yao, kuwasilisha maombi, na kupata taarifa zote muhimu kupitia simu au kompyuta zao bila kulazimika kufika ofisini. Hii imesaidia sana kupunguza muda wa kusubiri na kurahisisha upatikanaji wa huduma,” alisema Bw. Kijazi.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Modest Kilama, akizungumza wakati wa maadhimisho ya kilele cha wiki ya Tume hiyo jijini Dodoma, kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji Mstaafu Hamisa Hamisi Kalombola. Bw. Kilama alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za umma ili kuboresha utendaji na utoaji wa huduma kwa watumishi wa umma.
Alibainisha pia kuwa Mfuko umewekeza katika kuboresha miundombinu ya usalama wa taarifa za wanachama ili kuhakikisha kuwa faragha na usalama wa taarifa zao zinalindwa kwa kiwango cha juu zaidi. “Tunataka wanachama wetu wawe na amani ya akili wanapotumia huduma zetu za kidijitali, wakijua kuwa taarifa zao ziko salama.”
Kwa kumalizia, Bw. Kijazi alisisitiza kuwa mapinduzi ya kidijitali ndani ya PSSSF yanalenga kuboresha zaidi huduma kwa wanachama na kwamba ushirikiano kati ya PSSSF na Tume ya Utumishi wa Umma utaimarishwa zaidi ili kuleta matokeo chanya kwa watumishi wa umma.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Paul Kijazi, akizungumza na wadau mbalimbali wakati wa hafla ya maadhimisho ya kilele cha wiki ya Tume ya Utumishi wa Umma jijini Dodoma