
PSSSF YAPEWA TUZO YA KIMATAIFA
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Umepewa tuzo na Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Jamii (International Social Security Association-ISSA) kutokana na mafanikio iliyoyapata katika kipindi kifupi baada ya kuunganishwa (Merge) kwa mifuko minne ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF, PPF, GEPF NA LAPF na kuwa PSSSF
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Umepewa tuzo na Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Jamii (International Social Security Association-ISSA) kutokana na mafanikio iliyoyapata katika kipindi kifupi baada ya kuunganishwa (Merge) kwa mifuko minne ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF, PPF, GEPF NA LAPF na kuwa PSSSF.
Akizungumzia tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba, alisema sababu nyingine iliyoifanya ISSA kutoa tuzo kwa Mfuko huo ni pamoja na jinsi Mfuko ulivyoweza kupunguza gharama za uendeshaji na ulipaji wa mafao kwa wakati.
CPA Kashimba aliishukuru Bodi ya Wadhamini kwa usimamizi mzuri na hivyo kuufanya Mfuko huo kufanya vizuri.
“Kazi kubwa ya kusimamia zoezi hili la kuunganisha mifuko mmeifanya ninyi Bodi kwa maelekezo ya serikali, sehemu nyingi duniani wanasema karibu asilimia 85 ya kampuni zilizoungana huwa zinashindwa lakini muunganiko wetu sisi umeendelea kufanya vizuri hadi kuivutia taasisi hii kubwa kuifanya PSSSF kuwa mfano wa kuigwa.” Alisema CPA Kashimba.
Alisema tuzo hiyo ni zawadi kwa Bodi na sio Menejimenti pekee yake na Mfuko uko kwenye mikakati ya kuhakikisha unaendelea kutoa huduma bora kwa Wanachama wa Mfuko.
Akifafanua zaidi, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma (PSSSF) Bw. James Mlowe alisema PSSSF ilikabidhiwa tuzo hiyo jijini Abidjan Ivory Coast Mei 17, 2023 na Kwamba PSSSF inatarajia kufikisha miaka mitano tangu kuundwa kwake baada ya kuunganishwa kwa mifuko (merge).
“Majukumu ya mfuko yanatekelezwa vizuri, uwezo wa mfuko unazidi kuimarika, watumishi wanazidi kuwa kitu kimoja na kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kwakweli mafanikio haya ndiyo yamewavutia ISSA kuweza kutoa tuzo hii” Alisema